LIGI YA NSL YAENDELEA, TAMU CHUNGU ZATAWALA.
Hali mseto ziligubika nyuga mbalimbali za NSL nchini baada ya mechi anuwai za duru ya nane kusakatwa; idadi kubwa ya michuano ilichezwa wikendi iliyopita, huku nyingine kuchezwa siku ya Jumatatu. Baadhi ya klabu zilikuwa na nyoyo tulivu na zilizowanda baada ya kuwazidi wapinzani wao na kuchukua pointi zote tatu.
Shabana FC iliendeleza umafia wao kwa kufanikiwa kumaliza mchezo wake wa 7 katika duru ya kwanza kwa kuvuna alama tatu ugenini dhidi ya Naivas FC. Japo Naivas FC iliadhibiwa kwa kufungwa mara mbili, ni vizuri kuwapa kongole kwa kuweka rekodi murwa ya kuwa timu ya kwanza kabisa kutia mpira ndani ya wavu wa Shabana FC katika kinyang'anyiro cha kuvalishwa taji la NSL msimu huu. Mchuano huu wa Shabana na Naivas ulisisimua sana kwani timu zote mbili zilionyesha usanii mkubwa katika kusakata kabumbu. Timu ya Naivas iliweza kufungua ukurasa wa kutikisa nyavu mapema katika dakika ya 23 na kuweza kuzuia Shabana kufunga bao lolote hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.
Vijana wa Shabana hawakutamauka licha ya kufungwa bao la mapema; walikataa kabisa kuwa wendaguu; walijibiidisha zaidi na kuweza kusawazisha katika dakika ya 46, kipindi cha pili na hatimaye kupata bao la ushindi katika dakika ya 78 ya mchezo. Ushindi huo unahakikisha kuwa Shabana FC inasalia kileleni mwa jedwali ya NSL kwa alama 19, pointi 5 zaidi ya Kibera Black Stars wanaoshikilia nafasi ya pili.
Timu za Gusii FC, Coast Stima, Murang'a Seal na Darajani Gogo FC pia ziliweza kuvuna alama zote 3 za kung'ang'aniwa katika mchezo na kupunguza hali ya tumbo joto kwa wachezaji wao pamoja na benchi ya kiufundi wa klabu hizo baada ya kuwabwaga wapinzani wao. Transfoma za Coast Stima FC zilifanya kazi barabara kwa kuunguza na kuyeyusha bunduki za APS Bomet mara mbili ndani ya dakika tisini. Walinda sheria nao walishindwa kujibu uharibifu wa stima kwa kukosa kushika mitutu ya bunduki zao ipasavyo ili angalau wamimine hata risasi chache; walipigwa mabao mawili bila jibu.
Hadi sasa APS Bomet FC haina goli lolote wala pointi na hivyo basi Kipigo hiki kilizidi kutia ukungu na utusi katika azma yao ya kuamka na kushikilia nafasi ya juu kwenye jedwali kama walivyofanya msimu uliopita. Je, wataweza kugutuka na kufurahia tambaku kama walivyofanya msimu uliopita ama watavumilia utafunaji wa tambuu? Twasubiri kuona, bado ni macheo kufanya uamuzi wowote, tuzidi kupara samaki wetu, tulengete nyua zetu na tupepete mchele tukingojea machweo ndiposa tufanye maamukizi.
Kwingineko kule Ukunda, lililo geni lilishuhudiwa, ule msemo wa 'mcheza kwao utuzwa' haukuwa na mashiko yoyote, ufaafu wake ulikuwa ombwe tupu. Mwenyeji SS Assad FC alipokea kofi la usoni kutoka kwa Murang'a Seal FC; mgeni alifunga mara mbili nao wenyeji wakashindwa kufunga zaidi ya mara moja. Msomaji, mambo hayakuishia hapo.....shari kwa 'huyu' mara nyingine ni heri kwa 'yule'....
Vihiga United FC walikuwa ni wenye shari. Darajani Gogo FC walitembelewa na heri kwa kutia kikapuni mwao pointi tatu na magoli mawili bila kutaabishwa na joto la jua kali ya Mumias. Walimumunya 'mana' za 'walkover.' Hii ni kwa sababu Vihiga United walibanwa na uchefuchefu wa fedha jambo lililowafanya kutowajibikia ratiba ya mchuano kwa vile walishindwa kumudu gharama za nauli na zile za masurufu za wachezaji ikiwemo benchi ya kiufundi.
Mle ugani Serani Sports Ground wenyeji Mombasa Elites wakiisuluhisha na MCF FC walitoka sare ya kutofungana. Mtindo wa sare ya kutofungana uliigwa na timu ya Mara Sugar wakipambana na Migori Youth FC uwanjani Awendo Green Stadium. Kule Bomet, vijana wa nyumbani Silibwet Leons na Kisumu All Stars walitoka sare ya bao moja.
Wawakilishi wa kitingoji duni kubwa zaidi nchini Kibera Black Stars hawakuwa na dhima kuu ya kutekeleza wikendi iliyopita isipokuwa kufanya mazoezi ya kuwaivisha zaidi ya kuiva. Hii ni kwa sababu walipangwa kucheza na Fortune Sacco, timu ambayo inaaminiwa kuwa na maswala ya hapa na pale; tetesi zasema kuwa Fortune Sacco inashikilia kuwa inafaa kupandishwa daraja ili kucheza katika ligi kuu nchini.
NSL inaingia duru ya tisa, wikendi hii huku mechi mbalimbali zikiratibwa.Darajani Gogo FC itachuana na Mara Sugar FC, Gusii FC dhidi ya Naivas FC, MCF FC ipimane nguvu na Vihiga United, Murang'a Seal itaisuluhisha na Mombasa Elites FC, Kajiado FC itamenyana na Silibwet Leons FC, Kibera Black Stars wataisakata na Coastal Heroes FC. Pia, ubabe utakuwa unaamuliwa kati ya Kisumu All Stars na SS Assad FC kisha Migori Youth FC itacheza na Mwatate United FC.
Je, nani atakeyemzidi mwengine? Je, Shabana FC watazidi kupanua mwanya?